Vizuri Hupatikana Bure, Changamoto ni Kuvitambua

Jana kocha wako alipata furaha kubwa baada ya kutumiwa ujumbe na wamiliki ya mtandao wa kijamii wa picha sogezi wa YouTube kwamba chaneli yake iitwayo JasusiTV umefikisha waliojisajili (subscribers) 25,000.

Ukilinganisha na watu wengi maarufu, idadi hiyo ni kama tone kwenye bahari. Lakini kwa kocha wako anayeamini katika “nguvu ya mdogo mdogo”, hii ilikuwa habari kubwa sana kwake.

Na licha ya idadi ya waliojisajili kufikia 25,000 video ya mwisho hadi sasa imetizamwa na watu zaidi ya 50,000. Kwa kocha wako, hii ni idadi kubwa mno hasa kwa vile chaneli yake haijihusishi na ubuyu, kitu kinachopendwa zaidi na Watanzania.

Ubuyu umekuwa adui mkubwa sana kwa watu kama Kocha wako wanaojibidiisha kusambaza uelewa japo kiduchu walioanao.

Mara kadhaa kocha wako hutanabaisha kuwa uelewa ni kama fedha. Kwamba hata uwe na fedha nyingi kiasi gani, kama hazitumiki, hazina faida. Kadhalika, hata mtu awe na lundo la shahada na uelewa mkubwa, lakini kama uelewa huo hautumiki kwa manufaa ya jamii, hauna faida.

Sasa kocha wako ana uelewa sio hana, hususan kutokana na kiu yake kubwa ya kujifunza angalau kitu kimoja kila siku. Na mara kadhaa hutanabaisha kwamba njia mwafaka ya kujifunza ni kufundisha wengine. Ndio maana kocha wako hupendelea mno kufundisha na/au kushirikisha jamii kuhusu kidogo anachokielewa.

Hata hivyo, kupambana na ubuyu sio kazi rahisi kwa sababu inavunja moyo kuhangaika kuwashawishi watu wazima na akili zao kwamba hiki kidogo cha bure kutoka kwa kocha wako ni muhimu kuliko huo ubuyu unaolipia.

Lakini kama ilivyo vigumu kuwashawishi wapenda pombe kwamba kwenda nyumba ya ibada (kanisani/msikitini) hakuna gharama kulinganisha na kwenda baa, ndivyo ilivyo vigumu kuwashawishi wengi wenu kuhusu vitu muhimu vs ubuyu.

Kuna msemo kwamba “vizuri huwa bure”. Japo “bure” si lazima iwe “isiyo na malipo kabisa”, mara nyingi upatikanaji wa vitu vizuri huwa rahisi kuliko upatikanaji wa vitu vya ovyo.

Enewei, ikikupendeza, unaweza kumuunga mkono kocha wako kwa kujisajili kwenye chaneli yake iitwayo JasusiTV. Unaweza kujisajili HAPA

Kwaresma Njema na Ramadhan Njema kwa mliofunga.

Reply

or to participate.