- AdelPhil Online Academy
- Posts
- Wakati Mwingine Kutofanya Kitu Ni Kufanya Kitu Pia
Wakati Mwingine Kutofanya Kitu Ni Kufanya Kitu Pia
Msisitizo maishani umekuwa ni katika kufanya hiki au kufanya kile. Na kwa hakika msisitizo huo una faida lukuki. Kwa mfano, ili ufaulu, shurti usome kwa ajili ya maandalizi ya mtihani husika.
Na kama unataka kazi shurti uitafute na kutuma maombi ya kazi.
Na hata baraka na rehma za Mwenyezi Mungu zahitaji kufanya sala/dua.
Hata hivyo, kuna nyakati nyingi tu ambacho kitu unachopaswa kufanya ni kutofanya kitu chochote. Kwa mfano, kwenye mahusiano, hutokea wakati ambapo mwenza anatafuta ugomvi bila sababu. Ukiitikia wito wake, atapata anachokihitaji. Lakini ukiamua “kumwepuka shetani” na kutofanya chochote, yayumkinika kuamini kuwa kiu na anachokitafuta mwenza wako huyo itaisha yenyewe.
Mfano mwingine ni “vurugu za mtandaoni". Licha ya mazuri yake mengi, mtandao umetoa fursa kwa maharamia wengi tu kusumbua watu mtandaoni. Na mara nyingi huwalenga watu wenye umaarufu, kwa sababu, mtu maarufu akijibishana na haramia husika, inakuwa kama kumpiga teke chura. Njia mwafaka ni kutofanya anachohitaji haramia husika, yaani usipoteze muda kujibu upuuzi wake. Ofkoz bloku inaweza kutembea muda wowote ule endapo uharamia utazidi.
Lakini pia kuna nyakati ambapo unahitaji kutuliza akili. Na kama tunavyojua, ukifanya jambo lolote lile, akili inakuwa kazini. Sasa sio lazima hadi usubiri muda wa kulala ndio upumzishe akili. Miongoni mwa njia mwafaka ni kutulia tu bila kufanya lolote.
Ofkoz ni muhimu usiwe katika mazingira kama ya kazini ambayo yanahitaji uwe unafanya hili au lile. Mbinu hii ya kutulia bila kufanya chochote inaweza kuwa na ufanisi siku ambazo hukabiliwi na majukumu muhimu.
Reply